JAMII YANGU
LEO; katika Jamii yangu yangu, napenda nikulete habari juu ya jamii ya Wanyiramba
Kama zilivyo kwa jamii zingine za kibantu barani Afrika ambao walihamia Mashariki na Kusini mwa Afrika wakitokea Afrika Maghariki hususani nchi za Kameruni, Naijeria na Ghana wakipita misitu ya Kongo, Wanyiramba na Wanyisanzu walikuwa katika kundi mojawapo lililoelekea mashariki hadi maeneo ya Ziwa Nyanza (Victoria) hadi katika kisiwa cha Ukerewe kilichopo katika ziwa hilo kubwa zaidi barani Afrika. Japo haijulikani sababu hasa, kundi moja liliondoka kutoka katika kisiwa cha Ukerewe hadi Kisiwa cha Uzinza na kutoka hapo wakahama hadi maeneo ya Tabora ambako waligawanyiaka kundi moja likielekea kusini na inasemekana ndio waliokuja kuwa Wagogo na Wanyaturu huku kundi lingine likiendelea kuelekea Mashariki kupitia mlima Sekenke hadi Kisiriri.
Walipoanza kuitwa Wanyiramba na Wanyisanzu/Waihanzu Wakaishi hapo Kisiriri kwa muda mrefu kabla ya kutokea ukame mkubwa sana uliosababisha njaa katika eneo hilo. Ili kukabiliana na tatizo hilo la njaa, watu hao walitumia mboa za majani za mlenda uliokaushwa zijulikanazo kama "ndalu" kama chakula kikuu. Kutokana na kula "ndalu" kwa mtindo wa kulamba, watu wa makabila mengine ya kibantu walivyowaona wakawaita "wenye kulamba" na baadaye likabadilika hadi kuwa "wenyilamba" hadi "Wanyiramba". Ikumbukwe kuwa hadi hapo Wanyisanzu na Wanyiramba walikuwa kabila moja na wote walifahamika kama Wanyiramba baada ya njaa hiyo.
Wanyisanzu/Waihanzu wahamia pori la Mkalama Kundi moja likaamua kuondoka hapo Kisiriri hadi pori la Mkalama wakiwa na mifugo yao na familia zao na walipofika katika pori hilo ili kujilinda na wanyama wakali wakajenga nyumba na kuzungushia maboma ya miba maarufu kama "masanzu/mahanzu". Baadaye baadhi ya Wanyiramba waliobaki Kisiriri nao waliamua kuondoka hapo na walipofika Mkalama wakawakuta wenzao wamezungushia nyumba zao kwa Maboma ya "masanzu/mahanzu" ndipo walipoanza kuwaita hawa ni wanyisanzu au waihanzu.
Wanyiramba na Wanyisanzu japo wanahistoria inayofanana na kwa mtu mgeni anaweza kudhani kuwa hakuna tofauti baina yao, lakini ukweli ni kuwa kuna tofauti kubwa sana baina yao.
Koo zao na Wanapopatikana Wanyiramba Hizi ni koo tano za Wanyiramba na wanapopatikana
•Kinampanda: Wanaishi sehemu za milimani hasa huko Kinampanda •Anagimbu: Wapo Iramba Mashariki •Waiambi/waiyambi: Wanaishi Nkungi na Iambi •Anishai: Wanapatikana Kinandili na •Akimbu: Hawa wapo mpakani mwa Iramba na Tabora
Kwa upande wa Wanyisanzu, wao wana Koo nne tu
•Mnyakilumi: Wapo maeneo ya Kilumi/Kirumi •Mnyatumbili: Wanaishi Ikolo •Mnyadintima: Hawa wanapatikana Mwangeza na •Mnyasoha: Waishio Mkalama